Maafisa 6 wa chuo cha mafunzo ya kiufundi cha Thika wakamatwa Kwa kufuja shilingi milioni 27

Maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai wamewakamata maafisa sita wa chuo cha mafunzo ya kiufundi cha Thika kwa kufuja fedha za umma kupitia malipo yasiostahili ya kiasi cha jumla ya shilingi milioni 27,981,233. Idara ya upelelezi imesema kupitia mtandao wake wa Twitter kwamba washukiwa hao sita watafikishwa mahakamani leo.

Washukiwa hao ni pamoja na Mary Mumbua Kyengo Micheni, ambaye ndiye mkuu wa taasisi hiyo , Jefferson Kariuki- aliyekuwa mkuu wa zamani wa taasisi hiyo, John Mwangi ambaye pia alikuwa mkuu wa zamani chuo hicho, Samuel Gakuma aliyekuwa afisa wa masuala ya fedha, Johnson Kihumba Ichugu mkaguzi wa hesabu wa taasisi hiyo na Eunice Njuguna Wairimu mkaguzi wa hesabu wa wizara ya elimu huko Thika.

Ujumbe huo kupitia mtandao wa Twitter ulisema fedha hizo zilinuiwa kuimarisha uvumbuzi wa kiufundi wa teknolojia ya habari na mawasiliano. Taasisi hiyo imeteuliwa kuongoza katika uvumbuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano lakini fedha za wafadhili na serikali zilifujwa kwa matumizi ya kibinafsi.

Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa jinai George Kinoti ametoa onyo kali kwa taasisi nyingine za masomo hapa nchini akisema fedha za matumizi ya umma na hali ya siku za usoni ya watoto wa nchi hii sharti zilindwe na kutumiwa kwa malengo yaliokususdiwa.