Lusaka akosoa gavana Wangamati kwa kudhulumu wafanyikazi

Spika wa bunge la Senate, Ken Lusaka, amemshtumu gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati kwa madai ya kuwafuta kazi wafanyikazi wa kaunti walioajiriwa wakati wa muhula wake kama gavana wa kaunti hiyo. Lusaka ambaye aliongea huko Bungoma, alimlaumu gavana Wangamati kwa kuwadhulumu wafanyikazi wasio na hatia kwa sababu walimuunga mkono wakati wa uchaguzi mkuu ulliopita. Spika huyo wa bunge la Senate alisikitika kwamba wengi walioathiriwa na kufutwa kazi ndio wanaozikimu familia zao. Lusaka aliwaahidi wakazi wa Bungoma kwamba licha ya kupewa wadhifa wa spika wa bunge la Senate atakuwa akizuru eneo hilo kukamilisha miradi ya maendeleo alioanzisha alipokuwa gavana wa kaunti hiyo. Hata hivyo alipohojiwa kwa simu, mkurugenzi wa mawasiliano katika kaunti ya Bungoma, Timothy Chimatu, alipuuzilia mbali madai ya Lusaka akisema gavana wa sasa hana nia ya kumfuta kazi mtu yeyote. Mwanachama wa bodi ya utumishi wa umma ya Bungoma aliyeongea na shirika la utangazaji nchini-KBC kwa njia ya simu alisema bodi hiyo ilivunjiliwa mbali kabla ya muda wake wa kuhudumu kukamilika punde Wangamati alipochukua hatamu za uongozi. Suala hilo sasa limewasilishwa mahakamani ambako wanachama sita wa bodi hiyo wamepinga hatua ya kuivunjilia mbali bodi hiyo ya utumishi wa umma katika kaunti ya Bungoma.