Lusaka akanusha madai ya rushwa dhidi ya maseneta

Spika wa bunge la seneti Kenneth Lusaka amekanusha madai ya ulaji rushwa dhidi ya maseneta waliokuwa wakichunguza sakata ya ununuzi wa ardhi ya Ruaraka. Akiongea wakati wa mkutano wa kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu, Lusaka amemtaka yeyote aliye na ushahidi kuhusu madai hayo auwasilishe kwa wadau.

Siku ya Jumatatu mwenyekiti wa kamati ya uhasibu wa umma na uwekezaji Moses Kajwang alisema kwamba hana ufahamu wowote kuhusu madai yaliyotolewa na mfanyibiashara Francis Mburu kwamba baadhi ya maseneta waliitisha hongo ya shilingi milioni 100 kuhusiana na uchunguzi kuhusu sakata ya ardhi ya Ruaraka. Badala yake alimlaumu Mburu kwa kujaribu kubadilisha mtazamo wa kamati hiyo kwa kumtaka achunguzwe kwa kuuza ardhi ya umma baada ya kudai anaimili.