Linah Jebii Kilimo Ashtumu Mashambulizi Ya Kerio, Marakwet

Mwenyekiti wa kampeni ya kukabiliana na ukeketaji wa wanawake Linah Jebii Kilimo, ameshtumu mashambulizi yanayoendelea kwenye bonde la Kerio katika eneo bunge la Marakwet mashariki ambapo watu kumi wameuawa na maelfu ya mifugo kuibwa. Kilimo alizungumzia mashambulizi yaliyotekelezwa katika muda wa siku mbili zilizopita kwenye vijiji vya Kapen na Chesongoch na watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo wanaoaminika kuvuka mpaka kutoka kaunti za Pokot magharibi na Baringo ambayo yamesababisha vifo vya watu wawili. Akiwahutubia mamia ya wataalamu kutoka Marakwet waliokusanyika kwenye klabu cha Railways jijini Nairobi, kushtumu mashambulizi hayo, Kilimo aliihimiza serikali kuchukua hatua za haraka na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo. Akizifariji familia za wale waliouawa kwenye mashambulizi hayo waziri huyo msaidizi wa zamani alitoa wito wa kukomeshwa kwa uovu huo. Alitoa wito kwa wahisani kutoa chakula na mavazi kwa wakazi ambao alisema wanatoroka eneo hilo kutokana na ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama.