Ligi kuu ya Sportpesa kuendelea jinsi ilivyoratibiwa

Mechi ya kunyakua nafasi ya kushiriki katika ligi kuu ya Sportpesa msimu ujao, kati ya Thika United na timu ya Ushuru itaendelea kama ilivyoratibiwa hapo awali, baada ya tume ya kutatua maswala ya michezo humu nchini kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Thika United dhidi ya mechi hiyo.

Thika United ilimaliza ya kumi na sita katika ligi kuu ya Sportpesa, na kulingana na sheria za shirikisho la soka humu nchini, inatarajiwa kuchuana na timu ya Ushuru, iliyomaliza katika nafasi ya tatu katika ligi ya taifa msimu huu, huku mchuano huo ukiwa umeahirishwa mara mbili tayari hapo awali. Kulingana na uamuzi huo, Thika United pia inatarajiwa kulipa gharama ya kesi hiyo. Mkondo wa kwanza wa mchuano huo utandaliwa kesho, huku mechi ya mkondo wa pili ikiandaliwa siku ya Jumapili.