Lenny Kivuti apinga mahakami kuchaguliwa kwa Gavana Wambora

Seneta wa Embu anayeondoka Lenny Kivuti ambaye aliwania ugavana wa Embu amewasilisha rufani katika mahakama kuu akitaka kulindwa kwa vifaa vyote vya uchaguzi vilivyotumiwa kwenye uchaguzi wa ugavana huko Embu uliokamilika hivi punde ambapo alishindwa na Martin Wambora. Kwenye kesi iliyowasilishwa katika mahakama kuu ya Embu, Kivuti alisema vifaa hivyo vya uchaguzi vitatumiwa kama ushahidi kwenye rufani anayowasilisha akitaka kufutiliwa mbali kuchaguliwa tena kwa Wambora. Kupitia mawakili wake Tom Ojienda, Wilfred Nyamu na wengine Kivuti anataka karatasi zote za uchaguzi na fomu za matokeo katika maeneo bunge ya Manyatta na Runyenjes kuhifadhiwa na mahakama ili kuzuia kuvurugwa kwa ushahidi. Kwenye kesi hiyo iliyowasilishwa chini ya cheti cha dharura mbele ya jaji, Florence Muchimi, Kivuti alisema kucheleweshwa zaidi kwa kesi hiyo kunaweza kusababisha kuvurugwa kwa vifaa vya uchaguzi na washtakiwa. Kivuti anataka kura zote katika maeneo bunge hayo mawili kuhesabiwa tena na ulinzi wa vifaa hivyo vya uchaguzi utamsaidia kubatilisha ushindi wa Wambora.

Wambora alitangazwa mshindi kwenye uchaguzi mkuu siku ya Jumanne akiwa na kura 97,760 na kumshinda Kivuti ambaye alipata kura 96,775. Alisema maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC wametepetea katika kuwasilisha fomu za 37A na 37B za maeneo bunge hayo mawili na sasa Kivuti anaitaka mahakama kuwashinikiza kufanya hivyo. Gavana, Martin Wambora, tume ya IEBC na inspekta jenerali wa polisi wametajwa kama washtakiwa wa kwanza , pili na tatu mtawalio.