Kura za mchujo zaendelea kuhesabiwa huku Sonko akiongoza kaunti ya Nairobi

Kura zimeanza kuhesabiwa katika uchaguzi wa mchujo wa chama cha Jubilee katika kaunti ya Nairobi. Katika wadhifa wa ugavana seneta  Mike Sonko anaongoza kwa sasa kwa mujibu wa matokeo kutoka kwa baadhi ya maeneo bunge. Sonko aliongoza katika matokeo yaliyotolewa kutoka eneo bunge la Langata. Wakati huo huo mwaniaji wa tiketi ya ugavana ya chama cha Jubilee katika kaunti ya Nairobi Peter Kenneth amepinga matokeo ya mwanzo yanayotolewa kutoka vituo mbalimbali vya kupiga kura katika kaunti ya Nairobi huku akitaka shughuli hiyo kurudiwa kwa kutumia orodha sahihi ya wapiga kura.  Kenneth alitaka matokeo hayo kufutiliwa mbali akidai kuwepo kwa hitilafu kadhaa. Wakati huo huo matokeo ya mwisho kutoka kaunti ya Embu yametolewa huku gavana wa sasa wa kaunti hiyo Martin Wambora akitangazwa kuwa mshindi.  Wambora alizoa kura 60,549  na kumpiku mpinzani wake ambaye pia ni mbunge wa  Runyenjes  Cecily Mbarire alizoa kura  41,987. Na   Gladys Boss Sholei ambaye alikuwa msajili wa idara ya mahakama ameshinda shughuli ya uteuzi ya chama cha Jubilee ya kuwania wadhifa wa mwakilishi wa wanawake  katika kaunti ya Uasin Gishu. Sholei alimlaza  Janet Kurgat.  Mwakilishi wa sasa wanawake katika kaunti hiyo Eusila Ngeny  aliamua kutotetea wadhifa huo. Shollei alizoa kura 28,000 dhidi ya kura elfu tisa za Kurgat.