Kura yapigwa kinyume na msimamo wa Trump kutambua jiji kuu la Israel

Zaidi ya mataifa 120 yalipiga kura kinyume cha msimamo wa rais Donald Trump wa marekani wa kutambua Jerusalem kuwa jiji kuu la Israel, na badala yake kuunga mkono azimio la baraza kuu la umoja wa mataifa la kuitaka Marekani kubadii uamuzi huo. Trump alitishia kukatiza msaada wa kifedha kwa mataifa yatakayounga mkono azimio hilo. Jumla ya mataifa 128 yaliunga mkono azimio hilo , huku mataifa 9 yakipinga nayo mataifa 35 yakikosa kushiriki katika kura hiyo. Tishio la Trump lilionekana kuzaa matunda baada ya mataifa mengi kususia kupiga kura kuhusuu azimio hilo kando na awali ambapo mataifa mengi yenye uhusiano na Palestina yalionekana kuunga mkono azimio hilo. Hata hivyo, marekani imejipata imetengwa baada ya marafiki zake wa Uropa na Mataifa ya kiarabu kupiga kura kuunga mkono azimio hilo. Baadhi ya washirika hao ikiwemo misri, Jordan na Iraq, hupokea kiasi kikubwa cha misaada ya kijeshi au kiuchumi kutoka marekani ingawa tishio hilo la marekani la kukatiza misaada halikutaja nchi yoyote mahsusi. Msemaji wa mataifa ya magharibi yanayomuunga mkono rais Mahmoud Abbas wa wapalestina alitaja kura hiyo kuwa ushindi kwa palestina huku waziri mkuu wa Israel akipinga kura hiyo .