KUPPET Yatishia Kurejea Mahakma Dhidi Ya Mkataba

Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo-KUPPET kimetishia kuelekea mahakamani kuzuia mipango ya serikali ya kutathmini utendakazi wa walimu. Chama hicho kimesema serikali kupitia tume ya kuajiri walimu TSC haijashauriana kikamilifu na wadau husika. Naibu katibu mkuu wa chama cha KUPPET, Moses Nthurima amesema vyama vya KUPPET na KNUT havitakubali swala la kuwatathmini walimu hadi vitakapohusishwa kikamilfu katika shughuli hiyo. Nthurima pia amesema serikali ni sharti iongeze mishahara ya walimu kabla ya kuafikia makubaliano kuhusu swala la kusaini kandarasi za utendakazi. Wakati huo huo Nthurima ameshtumu serikali kwa kutowashughulikia walimu ipasavyo hususan swala la nyongeza ya mishahara na marupurupu ya walimu. Mthurima alisema hayo katika shule ya upili ya Wiyumiririe kaunti ya Laikipia wakati wa uchaguzi wa maafisa chama cha KUPPET tawi la kaunti hiyo.