Kukamatwa kwa Mwilu huenda ukaletea wadhifa wa naibu jaji mkuu matatizo

Wadhifa wa naibu jaji mkuu ambao kulingana na sheria unafaa kushikiliwa na mwanamke iwapo jaji mkuu ni mwanamme huenda ukakumbwa na matatizo ikizingatiwa matukio  yanayoshuhudiwa katika afisi hiyo.

Kukamatwa kwa naibu jaji mkuu Philomena Mwilu na kufikishwa mahakamani kunarejesha kumbukumbu za visa vya awali vilivyohusisha watangulizi wake. Mwilu ni naibu jaji mkuu wa tatu hapa nchini kukumbwa na utata .

Mnamo tarehe 31 Disemba mwaka 2011 aliyekuwa naibu jaji mkuu Nancy Baraza alituhumiwa kwa kumshambulia bawabu katika kituo kimoja cha kibiashara hapa jijini Nairobi. Jopo lililobuniwa wakati huo liliamua kuwa hafai kushikilia wadhifa huo na alilazimika kujiuzulu.

Mnamo tarehe 3 mwezi Juni mwaka  2013 hatamu ya Kalpana Rawal, aliyekuwa ameapishwa kuhudumu kwenye wadhifa huo ulikatizwa baada ya kutimiza umri wa kustaafu wa miaka  70 .

Umri wa miaka 70 ndio umri wa kustaafu kwa naibu jaji mkuu kulingana na uamuzi wa mahakama kuu lakini Rawal alipinga sharti hilo  . Hata hivyo rufaa yake ilifutiliwa mbali na mahakama ya rufaa.