KUDHEIHA chatetea hospitali ya Kenyatta kutokana na madai ya ubakaji

Chama cha wafanyikazi wa nyumbani, hoteli, taasisi za elimu, hospitali na taasisi husika (KUDHEIHA) kimeitetea hospitali ya kitaifa ya Kenyatta kuhusiana na madai ya ubakaji katika hospitali hiyo. Katibu mkuu wa KUDHEIHA Albert Njeru amesema madai hayo yanakera na yananuiwa kuwaharibia sifa wafanyikazi wa hospitali hiyo na hospitali hiyo kwa ujumbla. Akiongea na wanahabari, Njeru alisema chama chake kinawatafutaA�A�wanaoeneza uvumi huo kupitia kwa mitandao ya kijamii ili watoe ushahidi walio nao kuhusu madai hayo la sivyo chama hicho kiwachukulie hatua za kisheria. Njeru aliwataka wengine wanaodaiwa kubakwa kujitokeza na kuripoti kwa polisi. Aliongeza kusema kwamba hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ina wafanyikazi wa nidhamu ya juu na madai kama hayo ambayo hayajathibitishwa hayawezi kuvumiliwa.

Kufikia sasa hapana muathiriwa yeyote wa ubakaji ameandikisha taarifa kwa polisi licha ya miito ya waziri wa afya na wasimamizi wa hospitali hiyo ya kuwataka waandikishe taarifa kwa polisi. Wasimamizi wa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na chama cha madaktari wamekanusha madai hayo wakisema baada ya kutazama picha za video za usalama za hospitali hiyo wamebainisha kwamba hakuna kisa kama hicho kilitendeka hospitalini humo.