Korea Kaskazini yafanya majaribio kombora lake

Korea kaskazini imelifanyia majaribio kombora lake moja ambalo limeambaa kupitia anga ya kaskazini ya Japan kabla ya kutumbukia baharini. Japan haikufanya juhudi zozote kulitungua kombora hilo, huku hali ya wasi wasi ikisemekana kukumba sehemu hiyo. Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alilielezea tukio hilo kuwa tishio kubwa. Korea kaskazini imefanya majaribio mengi ya makombora yake lakini hili limekuwa la kwanza kupitia juu ya anga ya Japan. Siku za ijumaa na jumamosi taifa hilo lilirusha makombora matatu ya masafa mafupi kwenye mwambao wa mashariki wa bahari. Wakati kombora la leo lilipopitia juu ya anga ya kaskazini mwa Japan vyombo vya habari vya nchi hiyo vilitoa tahadhari japo hapakutokea uharibifu wowote kutokana na kombora hilo ambalo lilianguka baharini. Abe amelielezea jaribio hilo la kombora kuwa hatari kwa usalama wa kanda hiyo.