Kocha wa Crystal Palace Frank de Boer atishiwa kupigwa kalamu

Kocha wa Crystal Palace Frank de Boer anakabiliwa na tisho la kupigwa kalamu baada ya kupoteza mechi ya ligi kuu nchini Uingereza kwa mara ya nne mfululizo msimu huu na hivyo kuiacha timu hiyo bila alama ligini. Timu hiyo ilishindwa  bao 1-0 jana katika mechi ya ligi iliyochezwa katika uwanja wa Turf Moor. Palace ilijadilia uwezekano wa kumpiga kalamu kocha huyo wakati wa kipindi cha mechi za kimataifa  lakini ikaafikia uamuzi wa kumpa De Boer  fursa nyingine kuboresha matokeo ya timu hiyo. Iwapo kocha huyo atafutwa kazi basi huenda aliyekuwa kocha wa Palace na aliyeteuliwa hivi maajuzi mkurugenzi wa maswala ya michezo katika timu hiyo Dougie Freedman, atasimamia timu hiyo kwa muda. Palace   sasa ni timu ya kwanza inayoshiriki ligi kuu katika muda wa miaka 93, tangu Preston North End mwaka 1924, kupoteza mechi nne za mwanzo wa msimu bila kufunga bao. Timu hiyo imeshindwa na Huddersfield Town na Swansea City nyumbani na ugenini dhidi ya  Liverpool na  Burnley na kufungwa jumla ya mabao  7-0.