KNUT kutisha kukatiza kufunguliwa kwa shule mwezi ujao

Chama cha kitaifa cha walimu nchini kimetishia kukatiza kufunguliwa kwa shule mwezi ujao endapo tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC haitabatilisha hatua yake ya kuwahamisha walimu wengi wakuu wa shule mbali mbali za secondary na za msingi.Kwenye taarifa , Katibu mkuu wa KNUT Wilson Sossion aliwaagiza walimu wakuu ambao wamepewa uhamisho kupuuza barua za kuwahamisha walizotumiwa.Amesema chama cha KNUT kinapinga hatua ya kuwahamisha walimu wakuu 557.Alitaja hatua hiyo kuwa isiyofaa na inanuiwa kuwaathibu walimu hao wakuu.Sossion vile vile ameishutumu wizara ya elimu na tume ta TSC kwa kuchukua hatua kiholela bila kushauriana na vyama vya walimu huku akionya kwamba walimu watagoma endapo baadhi ya marekebisho yaliyofanywa hivi majuzi hayatabatilishwa.Afisa mkuu wa TSC Nancy Macharia amesema uhamisho huo wa baadhi ya walimu wakuu utakaoanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka ujao unanuiwa kuimarisha mshikamano wa kitaifa.Kulingana na TSC, hatua hiyo inakusudiwa kuleta mawazo mapya katika taasisi mbali mbali za masomo baada ya baadhi ya walimu wakuu kuhudumu katika taasisi zao kwa kipindi cha zaidi ya miaka tisa.Macharia alisema uhamisho huo utatekelezwa hatua kwa hatua.