KNEC Yaonya Kuwepo Kwa Makaratasi Bandia Ya Mtihani.

Mwenyekiti wa baraza la mitihani ya kitaifa la Kenya profesa George Magoha amekanusha madai kwamba mtihani wa mwaka huu wa kidato cha nne umeibwa.Professor Magoha amesema hakuna mtihani wowote umeibwa.Alikuwa akijibu ripoti zilizopokewa jana na baraza hilo kwamba kulikuwa na watu ambao walikuwa wakiuza makaratasi ya mitihani ya hisabati na Kemia iliyofanywa. Alisema kama ilivyokuwa wakati wa mtihani wa KCPE, makaratasi bandia ya mtihani huo yaliyokuwa yakiuzwa hayakuwa na uhusiano wowote na mtihani halali wa KCPE.Magoha aliwatahadharisha wazazi na walezi wajihadhari wasije wakalaghaiwa pesa na matapeli hao. Alionya kwamba wale wanaonunua makaratasi hayo bandia ya mitihani watawapotosha watoto wao ambao wametumia muda wao Mwingi kujiandaa kwa mtihani huo huku akiwanya kwamba watakamatwa kwa kujaribu kuiba mtihani.