Kizza Besigye Azuiliwa Nyumbani Kwake

Maafisa wa usalama nchini Uganda leo wamemzuia nyumbani kwake kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Kizza Besigye katika juhudi za kumzuia kuongoza maandamano huku raia wa nchi hiyo wakisubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Msemaji wa polisi nchini humo Fred Enanga alisema kwamba polisi walichukua hatua hiyo ili kuzuia kuzuka kwa fujo zaidi nchini humo. Polisi walizingira makao makuu ya chama cha Besigye cha Forum for Democratic Change,wakati kiongozi huyo alipokuwa akikutana na wanachama huku helikopta ya polisi ikifyetua gesi ya kutoa machozi kutawanya umati uliokuwa umekusanyika nje kabla ya kumtia nguvuni Besigye mwenye umri wa miaka 59.

Baadaye kiongozi huyo alirejeshwa kwake wakati wa usiku.Chama cha Besigye kimedai kumekuwa na wizi mkubwa wa kura uliotekelezwa na serikali hasa katika maeneo yenye wafuasi wengi wa upinzani. Na kuchochea ghasia.

Uchaguzi huo wa siku ya alhamisi ulikumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kucheleweshwa kwa makaratasi ya kura,ghasia pamoja na hatua ya serikali ya kufunga mitandao ya kijamii.

Matokeo ya hivi punde yameonyesha kuwa rais Museveni anaongoza kwa asili mia 60 ya kura huku Besigye akiwa na asili mia 35 ya kura.Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwaA� baadaye hii leo.Polisi waliwazuia wanahabari kukaribia nyumbani kwaA� Besigye mjiniA� Kampala.

Baada ya Besigye kutiwa nguvuni jana,wafuasi wake waliandamana kwenye barabara za mji wa kampala ambapo walikabiliana vikali na polisi.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Amerika ilisema waziri John Kerry alizungumuza kwa njia ya simu na rais Museveni akitaka kudumishwa kwa maadili ya kidemokrasia.Rais Museveni mwenye umri wa miaka 71 alichukua hatamu za uongozi nchini humo mwaka wa 1986.