Kivutha Kibwana arodheshwa kuwa gavana mwenye utendekazi bora na NPA

Ripoti ya kampuni ya utafiti ya NPA imemworodhesha gavana wa Makueni Prof. Kivutha Kibwana kuwa gavana mwenye utendakazi bora zaidi na kufuatiwa na gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru. Kwenye utafiti uliofanywa ili kutathmini siku 100 za magavana afisini , Kibwana ameorodheshwa bora zaidi kwa asilimia 55 huku Waiguru akiwa na asilimia 54 . Prof. Anyang’ Nyong’o wa Kisumu ameorodheshwa wa tatu kwa asilimia 53. Magavana wa kaunti za Narok na Vihiga Samuel Tunai na Wilbur Ottichilo wamekamilisha orodha ya magavana watano bora zaidi kwa asilimia 51 na 50 mtawalia. Hata hivyo utafiti huo unaashiria kuwa gavana Cyprian Awiti wa Homa Bay ameorodheshwa kuwa na utendakazi duni zaidi kwa asilimia 64 .Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameorodheshwa wa pili mwenye utendakazi duni zaidi kwa asilimia 61 huku magavana wa Mombasa, Garissa na Siaya wakiwa kwenye orodha ya magavana watano wenye utendakazi duni zaidi wote kwa asilimia 58. Utafiti huo ulioandaliwa kati ya tarehe nane na kumi Disemba umebainisha kuwa asilimia 43 ya wakenya wameridhishwa na jinsi magavana wanavyofanya kazi yao huku asilimia 51 wakikosa kuridhika.