kituo cha utoaji damu kwa ajili ya manusura wa ajali chazinduliwa Kericho

Hospitali ya matibabu maalum ya Kericho imezindua kituo cha utoaji msaada wa damu kwa lengo la kuwasaidia manusura wa ajali ya barabarani iliyotokea jana asubuhi na kusababisha vifo vya abiria 56. Gavana wa kaunti ya Kericho Paul Chepkwony amesema manusura wa ajali hiyo waliolazwa katika hospitali hiyo wanahitaji matibabu ya kina ukiwemo upasuaji na watahitaji kuongezwa damu. Gavana Chepkwony alielezea wasiwasi wake kuhusu uhaba wa damu katika hifadhi ya hospitali za kaunti hiyo.

Wakati huo huo, Polisi wamemtia mbaroni mmiliki wa lile basi lililohusika kwenye ajali mapema jana asubuhi na kusababisha vifo vya abiria 56 huko Kericho. Bernard Ishindu Shitiabayi,mmiliki wa basi hilo almaarufu Home Boyz linalosimamiwa na Western Cross Express Sacco, alikamatwa jana jioni mjini Kakamega.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kericho James Mugera aliliambia shirika la utangazaji la KBC kwa njia ya simu kuwa Shitiabayi alikamatwa pamoja na Cleophas Shimanyula wa Western Cross Express Sacco.