Kipindupindu yaua 3 Tharaka Nithi

Watu watatu wamefariki na wengine 71 kulazwa katika hospitali mbali mbali kaunti ya Tharaka Nithi kufuatia chamuko la ugonjwa wa kipindupindu. Akiongea na wanahabari, afisa mkuu wa afya katika kaunti ya Tharaka Nithi, Gidhuyia Nthuraku alisema ugonjwa huo huenda ulisababishwa na maji machafu kutoka kwa miito. Alisema serikali ya kaunti hiyo imechukua hatua zote kukabiliana na ugonjwa huo ambao umeendelea kusababisha madhara makubwa.

Wakati huo huoA�alitoa wito kwa wakazi kujitunza wanaposhughulikia chakula na kutumia maji safi yaliyochemshwa. Afisa huyo wa afya pia amepiga marufuku uchuuzi wa chakula katika kaunti hiyo. Nalo shirika la msalaba mwekundu, limeingilia kati kuthibiti ugonjwa huo kwa kutoa shehena ya dawa na vifaa vya kusaidia kukabiliana na chamuko hilo.

Mwezi Oktoba mwaka uliopita, watu wawili walifaiki ilhali wengine 26 walilazwa hospitalini katika kaunti jirani ya Embu kufuatia chamuko la ugonjwa wa kipindupindu. Dalili za ugonjwa wa Kipindupindu ni kuharisha zaidi ya mara nne katika muda wa saa 12. Hii inafuatia na upungufu mkubwa wa maji mwilini hali ambayo inaweza kusababisha kifo ikiwa matibabu hayatapatikana haraka.