Kiongozi Wa Vijana Wa Mrengo Wa ODM Kaunti Ya Nairobi Stephen Mukabana Auwawa

Mwanasiasa mmoja wa chama cha ODM aliuawa kwa kupigwa risasi jana usiku kwenye lango la nyumba yake katika eneo la Ruai jijini Nairobi. Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Kayole, Ali Nuno alithibitisha kuwa Stephen Odongo Mukabana mwenye umri wa miaka 42 alishambuliwa alipokuwa akisubiri lango la nyumba yake kufunguliwa katika mtaa wa Chokaa. Ilidaiwa Mukabana alishambuliwa na wanaume sita, mmoja wao akiwa amejihami kwa bunduki ambao walimpiga risasi kichwani na kwenye tumbo. Washambulizi hao waliiba kifuko chake cha pesa kikiwa na kiasi kisichojulikana cha pesa na simu yake ya rununu lakini wakaacha gari lake aina ya Toyota Prado mahali hapo. Polisi wamewakamata washukiwa kadhaa akiwemo David Wainaina Njoroge ambao wanazuiliwa kwa uchunguzi. Mukabana ambaye alikuwa kiongozi wa vijana katika kaunti ya Nairobi pia alikuwa mwenyekiti wa kundi la vijana la Bamaho ambalo linahusika na ununuzi na uuzaji wa mashamba katika eneo la Njiru jijini Nairobi.