Kikao Cha Jumuia Ya Afrika Kigali, Rwanda Chaahirisha Uchaguzi Wa Mwenyekiti Mpya Wa Tume Ya Jumuia Hiyo

Kikao cha Jumuia ya Afrika mjini Kigali, Rwanda kimeahirisha uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa tume ya jumuia hiyo baada ya wawaniaji watatu kukosa kupata idadi ya kura zinazohitajika. Hii ni baada ya viongozi kutoka nchi wanachama wa shirika la ECOWAS kukataa kushiriki kwenye uchaguzi huo baada ya pendekezo lao la kuwasilisha mwaniaji kukataliwa. Wawaniaji hao walitarajiwa kumrithi mwenyekiti wa tume ya jumia ya Afrika anayeondoka, Nkosazana Dlamini-Zuma. Wawaniaji hao walikuwa ni pamoja na Specioza Wandira ambaye ni makamu wa rais wa zamani wa Uganda, waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Botswana, Pelonomi Venson na mwenzake wa Equatorial Guinea, Agapito Mokuy. Kwa mujibu wa kanuni za jumuia ya Afrika, mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa tume ya jumuia hiyo wanachaguliwa na viongozi wa nchi na serikali ama waakilishi wao kwenye mkutano huo, ilihali makamishna wanane wa tume hiyo huchaguliwa na mawaziri wa mashauri ya nchi za kigeni kutoka nchi wanachama