Kiangazi Chakumba Baringo

Hali ya kiangazi imekumba maeneo kame ya kaunti ya Baringo ambapo wakazi wanatatizika kupata maji na lishe ya mifugo wao. Maelfu ya wakazi wa maeneo ya Mogotio, Tiaty na Baringo ndio walioathiriwa zaidi huku baadhi yao wakichimba visima na wengine wakilazimika kusafiri mwendo mrefu kutafuta maji. Mifugo nao wamekosa lishe na kulazimika kutafuna majani ya miti, hali ambayo imewafanya wengi wao kufariki huku wenyewe wakiwachinja wengine ili kuepuka hasara. Katika eneo la Barwesa, kaunti ndogo ya Baringo Kaskazini, wafugaji wanakadiria hasara kubwa bada ya mifugo wao kuangamia kutokana na ukosefu wa lishe. Wakazi hao wametoa wito kwa serikali za kaunti na taifa kununua mifugo hao ili kuepusha hasara zaidi.