KFS Yaeleza Wasiwasi Kuhusu Ongezeko La Biashara Ya Magendo Kwale

Shirika la huduma za misitu nchini-(KFS), limeelezea wasi wasi wake kuhusu ongezeko la biashara ya magendo inayohusisha makaa katika eneo la mpakani la Lunga Lunga, Kaunti ya Kwale. Mkurugenzi wa (KFS) katika Kaunti ya Kwale, Nafasi Mfahaya amesema magendo ya bidhaa hiyo huendeshwa usiku na magenge ya wale wanaoingiza humu nchini shehena kubwa ya makaa kutoka Tanzania kupitia kwenye mto Umba. Alisema mauzo ya makaa ugenini yamepigwa marufuku nchini Tanzania, na ndio sababu wahusikaA� wa biashara hiyo ya magendo wameamua kuendesha biashara yao nyakati za usiku. Pia alisema iwapo hatua mwafaka hazitachukuliwa, nchi hii itaendelea kupoteza fedha za ushuru, kutokana na hali ya wafanyibiashara hao kukwepa kulipa ushuru. Mfahaya alikuwa akihutubia kongamano la uhamasisho kwenye hoteli moja ya Mombasa kuhusu wajibu wa bunge la Afrika mashariki katika mpango wa utangamano wa nchi za Afrika mashariki. Mwaka uliopita, Kenya na Tanzania zilitia saini mkataba wa miaka mitano kuangazia hatua za ushirikiano kwa lengo la kudhibiti rasilimali za misitu, hususan maswala ya forodha ili kuangamiza magendo ya bidhaa za mbao na makaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *