Keriako Tobiko Kukata Rufaa Dhidi Ya Washukiwa Wa Ufisadi Wa Ubalozi Wa Kenya Mjini Tokyo

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko, amesema atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa kumuondolea aliyekuwa katibu katika wizara ya mashauri ya Kigeni Thuita Mwangi mashtaka ya ufisadi kuhusiana na ununuzi wa ardhi yaA� ujenzi wa jumba la ubalozi wa Kenya mjini Tokyo, Japan. Tobiko amesema hakimu alikosea kuwaondolea mashtaka washukiwa wote kwa msingi upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha dhidi yao. Mwangi na washtakiwa wenza wawili A�waliondolewa mashtaka yote kuhusiana na ununuzi tata wa ardhi ya ujenzi wa ubalozi wa Kenya mjini Tokyo Japan kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5.A� Wakili wao, Paul Muite, alisema uamuzi huo wapasa kutuma ishara dhahiri kwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi na mkurugenzi wa mashtaka ya umma kwamba walifanya uchunguzi duni. Mwangi alikuwa ameshtakiwa pamoja na naibu wa mkurugenzi wa masuala ya usimamizi Anthony Mwaniki Muchiri na aliyekuwa afisa mkuu wa kibalozi katika ubalozi wa Kenya mjini Tokyo Allan Waweru Mburu. Wote walikanusha mashtaka hayo.