Kenyatta, Trump washauriana katika Ikulu ya White House

Rais Uhuru Kenyatta ambaye yuko ziarani nchini Marekani  alifanya mashauriano na mwenyeji wake rais Donald Trump katika Ikulu ya rais,mjini Washington DC.Kikao cha Rais Kenyatta na mwenyeji wake Rais Trump katika Ikulu ya White House, kilimulika  zaidi biashara, uekezaji na usalama.Rais Uhuru aliomba nchi ya Marekani kuongeza zaidi biashara na uekezaji wake katika bara la Afrika.

Viongozi hao wawili walikubaliana kuimarisha ufungamano wa Kenya na Marekani katika udumishaji wa amani na usalama hasa katika eneo la upembe wa Afrika.Rais uhuru alisema  Kenya na Marekani  zimekuwa na ushirikiano mzuri na wa kipekee katika masuala ya usalama na ulinzi, hasa katika harakati za kukabiliana na ugaidi,huku akisema kusudi la ziara yake ni kuboresha ufungamano  katika biashara na uekezaji.

Viongozi hao wawili walijadiliana kuhusu safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York zitakazoanza mwezi Oktoba mwaka huu na kukubaliana kwamba zitaimarisha zaidi utalii na biashara kwa manufaa ya nchi hizi mbili.Aidha walitoa mfano wa Mkataba wa Nafasi na Ustawi wa Afrika maarufu kama Mkataba wa  kama moja wapo wa nyanja zitakazonufaika na  safari hizo za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi.

Pembezoni mwa mkutano huo mama wa taifa Margaret Kenyatta  na  mke wa rais wa Marekani Melania Trump walifanya mashauri ya faragha katika chumba cha masuala ya kidiplomasia katika Jengo la White House.