Kenya yasisimua wengi kwenye mbio za marathon jijini London

Wanariadha wa humu nchini Mary Keitany na Daniel Wanjiru jana waliibuka washindi wa mbio za marathoni za jijini London kitengo cha wanawake na wanaume mtawalia.. Mary Keitany, aliye na umri wa miaka 35 aliandikisha rekodi mpya duniani kwenye mbio za akina dada katika muda wa  saa mbili  dakika 17 na sekunde moja. Keitany aliondoa takriban sekunde 41 kwenye rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na mwanariadha wa nchini Uingereza  Paula Radcliffe tangu mwaka 2003. Keitany ambaye pia ametwaa mbio za marathoni za New York mara tatu alimpiku  Tirunesh Dibaba wa Ethiopia aliyemaliza wa pili katika muda wa saa mbili dakika  17 na sekunde 56 hii kiwa ni rekodi mpya ya kitaifa nchini humo. Aselefech Mergia wa Ethiopia  alimaliza wa tatu huku bingwa wa Olimpiki, mbio za mita elfu tano, Vivian Cheruiyot akimaliza wa nne katika muda wa saa mbili dakika 23 na sekunde 50 hii ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika mbio za marathoni. Mkenya Daniel Wanjiru aliibuka mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanaume katika muda wa saa mbili  dakika tano na sekunde  50 na kujishindia taji yake ya kwanza ya mbio za marathoni zenye hadhii kuu. Kenenisa Bekele alimaliza wa pili naye  Bedan Karoki aliyekuwa pia akishiriki katika marathoni kwa mara ya kwanza akimaliza wa tatu.