Kenya Yashuka kwenye orodha ya FIFA

Kenya imedondoka nafasi 12 hadi katika nafasi ya 115 kwenye orodha ya shirikisho la soka duniani FIFA. Rekodi ya matokeo duni pia imeifanya Kenya kushuka hadi katika nafasi ya 33 Barani Afrika.A�A� Baada ya msururu wa matokeo duni ya timu ya taifa ya Kenya katika mechi za kimataifa, Harambee Stars imedondoka nafasi 12 kwenye orodha ya shirikisho la soka duniani FIFA, na sasa inashikilia nafasi ya 115 kwa alama 303 pekee.

Aidha, matokeo hayo yameiwacha Harambee Stars katika nafasi ya 33 barani Afrika, alama 468 nyuma ya timu bora barani Afrika, Aljeria. Kenya imeshindwa kuandikisha ushindi katika mechi zake za kufuzu kwa fainali za kombe la dunia na zile za Bara Afrika na haina matumaini ya kucheza katika fainali zijazo za viwango hivyo.

Ajentina imechupa kileleni pa orodha hiyo, mbele ya Ubelgiji huku Chile, Kolombia na Ujerumani zikifunga orodha ya timu tano bora duniani. Aljeria ndio timu bora barani Afrika mbele ya Kodivaa, Ghana, Senegali na Misri zinazofunga orodha ya timu tano bora. Uhispania inashikilia nafasi ya sita, Brazil ni ya saba nayo Uingereza iko katika nafasi ya kumi.