Kenya Imeshuka Kwa Nafasi 6 Katika Kiwango Kipya Cha Nchi Fisadi Duniani

Kenya imeshuka kwa nafasi sita katika kiwango kipya cha nchi fisadi duniani kilichotolewa na shirika la Transparency international-TI hadi nafasi ya 145 duniani ikilinganishwa na nafasi ya 139 hapo mwaka wa 2015. Nchi zilizoorodheshwa nafasi ya 145 pamoja na Kenya ni Bangladesh, Cameroon, Gambia, Madagascar na Nicaragua. Utafiti huo unasema kuwa Kenya inasafari ndefu licha ya kufikia hatua kadhaa za kupambana na ufisadi zikiwemo kupitishwa kwa sheria kuhusu haki ya kupata taarifa. Shirika la TI limesema Kenya inahitaji mikakati mipya ya kupambana na ufisadi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuelezea anavyotatizika baada ya juhudi zake za kupambana na ufisadi kukumbwa na changamoto. Kulingana na uchunguzi wa kila mwaka wa shirika la Transparency International Somalia, Sudan Kusini, Korea kaskazini na Syria zinachukuliwa kuwa nchi fisadi sana duniani. Hata hivyo mataifa ya Ulaya ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na ufisadi wa kiwango cha juu zikiwemo nchi nne kati ya tano zilizo kwenye nafasi za juu. Denmark na New Zealand ndizo nchi safi duniani zisizokumbwa na ufisadi zikifuatiwa na Finland, Sweden na Switzerland. Katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika, Botswana ilitajwa kuwa nchi isiyokumbwa A�na visa vingi vya ufisadi ikiwa katika nafasi ya 35 ikifuatiwa na Cape Verde, Mauritius, Rwanda na Namibia. Aidha shirika la TI lilisema nchi zaidi kote duniani zilishuka badala kuimarika katika matokeo ya mwaka huu na kuonyesha haja ya dharura ya hatua ya kujitolea kukabiliana na ufisadi. Baadhi ya nchi za kiafrika zilizoshindwa kuimarisha juhudi za kupambana na ufisadi ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria, na Tanzania. Transparency International imesema nchi za Afrika zilizo kwenye nafasi za chini kwenye kiwango hicho cha ufisadi zinakumbwa na ufisadi, utawala mbaya na taasisi hafifu.