Kaunti Ya Vihiga Yapokea Kliniki Maalum Kutoka Kwa Mama Wa Taifa

Mama wa taifa Margaret Kenyatta amewashukuru wakenya kwa kuunga mkono kampeni yake ya Beyond Zero kwa kusaidia kukusanya pesa za kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya za kina mama na watoto. Alisema kuwa kupitia nia yao njema na ile ya serikali ya kitaifa na zile za kaunti na pia sekta ya kibinafsi ameweza kuwasilisha kliniki 41 maalum. Kliniki hizo zinanuiwa kuwasilisha huduma za afya karibu na jamii ili kupunguza vifo vya kina mama na watoto.

Mama wa taifa aliyasema hayo jana alipokabidhi kliniki ya 41 maalum kwa kaunti ya Vihiga. Kliniki hiyo ilitolewa na shirika la Rotary International. Ingawa ufanisi mkubwa umeafikiwa katika kupunguza visa vya maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa kina mama hadi kwa watoto, mama wa taifa alisema kuwa idadi kubwa ya kina mama wajawazito nchini bado hawapati huduma za kabla na baada ya kujifungua.