Kaparo apuuzilia mbali wakosoaji wanotaka tume ya NCIC ivunjwe

Mwenyekiti wa tume ya maridhiano na mshikamano wa kitaifa, NCIC Francis Ole Kaparo, amewapuuzilia mbali wakosoaji wake wanaotaka tume hiyo ivunjwe kwa kukosa kuwashitaki wanasiasa kwa kutoa hotuba za chuki. Kaparo jana alisema hatashinikizwa kumkamata au kumshitaki mtu yeyote. Alisema tume ya NCIC hufuata taratibu za sheria na hivyo haiwezi kukamata au kushitaki yeyote kiholela. Haya yanajiri huku wanasiasa na wanaharakati wa haki za binadamu wakitoa wito kwa kuvunjwa kwa tume hiyo. Siku ya Ijumaa, mtetezi wa haki za binadamu Al-Amin Kimathi na seneta wa Mombasa, Mohamed Faki, walisema tume hiyo inapaswa kuvunjwa, wakiitaja kuwa isiyokuwa na mamlaka na ambayo imeshindwa kuwachukulia hatua wanaoeneza chuki. Kimathi na Faki walisema tume hiyo inatumia pesa za walipaji ushuru bila kuleta mafanikio yoyote. Walitoa mfano wa matamshi ya mbunge wa Gatundu kusini, Moses Kuria na gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ya siku ya jumanne. Yadaiwa wawili hao wakiwa kwenye mkutano wa kisiasa wa kupigia debe kuchaguliwa kwa rais Uhuru Kenyatta, walitoa matamshi ambayo yalichukuliwa na upinzani kuwa hotuba ya chuki. Inasemekana Kuria alisema wako tayari kwa uchaguzi mwingine lakini watawasaka watu ambao hawakumchagua Uhuru.A� Aidha inadaiwa aliahidi kuwasaka wafuasi wa Raila Odinga huko Kiambu. Katibu mkuu wa chama cha Jubilee Raphael Tuju alisema matamshi hayo hayafai.