Kanda za video hazitatumiwa katika mechi za ligi ya kilabu bingwa barani Ulaya

Kanda za video zinazowasaidia marefa kufanya uamuzi michuanoni hazitatumiwa katika mechi za ligi ya kilabu bingwa barani Ulaya msimu ujao huku kinara wa UEFA akisema zinaleta utata michuanoni. Bodi inayosimamia mashirikisho ya soka duniani, na inayofanya uamuzi wa sheria za soka, itaandaa kikao siku ya Jumamosi kuamua iwapo teknolojia hio itatumiwa michuanoni. Iwapo itaamua itumike, basi shirikisho la FIFA litalazimika kutumia kanda hizo wakati wa fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi Juni.

Wakati uo huo kilabu cha Italia, Atalanta, kitachunguzwa na shirikisho la UEFA kwa madai ya ubaguzi wa rangi wakati wa mechi ya ligi ya YuropaA�A�dhidi ya Borussia Dortmund juma lililopita. Mshambulizi wa Chelsea Michy Batshuayi, anayeichezea Dortmund kwa mkopo, alisema alibaguliwa na mashabiki wa Atalanta wakati wa mechi hiyo ya raundi ya 32 bora nchini Italia. Kamati ya nidhamu ya UEFA itafanya uamuzi wa kesi hiyo tarehe 22 mwezi ujao. Batshuayi alicheza dakika tisini za mchuano huo siku ya Alhamisi ambapo mchezaji wa akiba Marcel Schmelzer alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 82 na kuiwezesha Dortmund kufuzu kwa raundi ya 16 bora kwa jumla ya mabao 4-3