Kamishna Wa Kaunty Ya Mandera, Fredrick Shisia Aondolea Mbali Hofu Dhidi Ya Mashambulizi Ya Al-Shabaab Mandera

Kamishna wa kaunty ya Mandera Fredrick Shisia ameondolea mbali hofu kwamba kundi la Al Shabaab linapanga kutekeleza mashambulizi katika sehemu hiyo. Hii inafuatia ripoti kutoka kwa wananchi kwamba kundi la wapiganaji wapatao 40 wa Al Shabaab limevuka mpaka na kuingia mjini Mandera. Alisema kwa njia ya simu kuwa habari hizo ni za uongo na kwamba maafisa wa usalama wanashika doria mpakani.

Shisia amewasiliana na wasimamizi wa eneo jirani la Bulahawa nchini Somalia na kuhakikishiwa hakuna wahalifu wamevuka mpaka hadi Mandera. Siku ya ijumaa polisi walipata risasi 540 kutoka kwenye mjengo mmoja mjini humo na baadaye kilipuzi kimoja kilichokuwa kikiwalenga maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria kikalipuka karibu na afisi ya ushuru wa forodha ya Kenya. Hakuna aliyeripotiwa kuuawa au kujeruhiwa.