Viongozi Wataka Kampuni Zinazotayarisha Pombe Duni Zifungwe

Viongozi kutoka kaunti  11 katika eneo la kati wanataka kampuni  115 za pombe ambazo bidhaa zao zilibainika kutotimiza viwango vya ubora vinavyohitajika wakati wa msako wa mwaka uliopita zifungwe kabisa.

Aidha viongozi hao wanataka bidhaa  21 za pombe zilizobainika kufaa  kwa matumizi ya binadamu zifanyiwe majaribio zaidi na kampuni ya kimataifa ya ukadiriaji ubora wa bidhaa ili kuhakikisha eneo hilo halina pombe hiyo.

Hayo yamejiri huku viongozi waliojumuisha magavana , maseneta , wanachama wa bunge la kitaifa na lile la kaunti na maspika wao wakikamillisha mkutano wa siku mbili ambapo maswala muhimu yanayohusu eneo hilo yalijadiliwa.

Waziri wa ugatuzi  Mwangi Kiunjuri, seneta wa Meru Kiraitu Murungi, seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe na gavana wa Laikipia John Irungu ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria mkutano huo .