Kamati Ya Pamoja Kuhusu Tume Huru Ya Uchaguzi Na Mipaka Haijakamilisha Ripoti

COTU

Kamati ya pamoja kuhusu tume huru ya uchaguzi na mipaka bado haijakamilisha ripoti yake kuhusu marekebisho yanayopswa kutekelezwa kwenye tume hiyo. Kufikia Ijumaa iliyopita, kamati hiyo inayojumuisha wanachama wa mirengo ya Jubilee na CORD ilikiwa imeafikiana kuhusu baadhi ya mapendekezo kuhusiana na marekebisho kwenye tume hiyo.

Muda uliotolewa kwa kamati hiyo wa kukamilisha ripoti yake na kuwasilisha mapendekezo ulitamatika ijimaa iliyopita. Hata hivyo inaonekana kana kwamba kamati hiyo imeshindwa kuafikiana na ripoti yake bado haijakamilika. Duru zinadokeza kuwa wanachama wa kamati hiyo wanakinzana kuhusu masuala muhimu yanayohusiana na tume hiyo hususan suala la idadi ya makamishna wanaopaswa kuhudumu kwenye tume hiyo na masharti yao ya kuhudumu.

Inaaminika kuwa mrengo wa Jubilee unapendelea tume ya makamishna tisa wa kudumu ilhali mrengo wa CORD unapendekeza makamishna 5 watakaohudumu kwa kandarasi za muda mfupi. Inaaminika kuwa wanakamati hao sasa wanashauriana na viongozi wa mirengo hiyo miwili ili kutafuta suluhu kwa suala hilo.