Kamati Ya Bunge Kuhusu Masuala Ya Sheria Yapokea Rufani Inayohimiza Makamishna Wa IEBC Watimuliwe

Kamati ya bunge la taifa kuhusu haki na masuala ya sheria imepokea rufani inayohimiza kutimuliwa kwa makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC. Rufani hiyo iliyowasilishwa na Barasa Nyukuri inaelezea jinsi makamishna wa sasa wameshindwa kudumisha uadilifu wa tume ya IEBC na hivyo basi wapasa kuondolewa ofisini. Kulingana na rufani hiyo miongoni mwa kasoro nyingine ambazo zimekumba tume ya uchaguzi ya sasa ni pamoja na kuendelea kushindwa kuwasajili wapiga kura na kukagua sajili za wapiga kura kama inavyohitajika kisheria. Mwasilishi wa rufani hiyo pia anahoji uhuru wa tume ya uchaguzi, akisema ilipokea maagizo kutoka kwa serikali wakati wa kugawana vifaa vya uchaguzi na Burundi. Nyukuri ambaye ni wakili pia ametahadharisha bunge dhidi ya kutumia kamati mpya iliyobuniwa ya mahauriano kuondoa tume ya IEBC akisema hatua kama hiyo inaweza kukumbwa na kesi nyingi.