Kajiado Magharibi Yanufaika Na Uzinduzi Wa Mradi Wa Huduma Kwa Vijana

Waziri wa utumishi wa umma na masuala ya vijana na jinsia Sicily Kariuki amekariri kujitolea kwa serikali kuwawezesha vijana kujimudu maishani. Kariuki alitaja miradi ya shirika la vijana wa huduma kwa taifa-NYS ambayo imezinduliwa upya kama mojawapo ya njia ya kuwashirikisha vijana katika ujenzi wa taifa. Kariuki aliwahimiza viongozi wa kisiasa kuendelea kuunga mkono miradi hiyo.Eneo la Kajiado magharibi ndilo la hivi punde kunufaika na uzinduzi wa miradi hiyo inayosimamiwa na wizara ya masuala ya vijana. Viongozi wa eneo hilo walisifu uzinduzi wa miradi hiyo na wakawahimiza wakazi kushiriki kwa wingi ili kujiimarisha kiuchumi. Miradi hiyo ilikwama mwaka jana baada ya shirika la NYS kukumbwa na kashfa za ubadhirifu wa pesa ambapo baadhi ya maafisa wa ngazi za juu wa shirika hilo waliachishwa kazi.