Justin Muturi Asema Bunge Limejitolea Kikamilifu Kurekebisha Sheria Za Uchaguzi

Spika wa bunge la kitaifa , Justin Muturi,amesema bunge limejitolea kutekeleza kikamilifu jukumu lake katika kurekebisha sheria za uchaguzi.Spika hata hivyo alitoa changamoto kwa wakenya kuwasilisha maombi kwa bunge kuhusu masuala wanayolitaka lishughulikie. Muturi alisema ni muhimu kwa vyama vya kisiasa kushauriana na wananchi na kubadilishana mawazo kuhusu marekebisho mbali mbali ya shughuli za uchaguzi ambayo yataiwezesha nchi hii kuimarisha demokrasia.Alisema hayo jana alipowaandalia wanachama wa chama cha wahariri kifungua kinywa ambapo vyombo vya habari vilihimizwa kuandika habari kwa uwajibikaji na uadilifu ili kuepuka kuitumbukiza nchi hii katika ghasia.Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya haki na masuala ya ksheria, Samuel Chepkonga, alitoa wito wa uadilifu katika kushughulikia mzozo wa tume ya IEBC akisema kamati yake iko tayari kuwasilisha bungeni mswada wa marekebisho ya tume hiyo utakaowezesha uteuzi wa makamishna wake kuwashirikisha wote.
Wakati huo huo kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa , Aden Duale,alivitaka vyombo vya habari kuandika habari za manufaa kwa nchi hii na kusaidia kuilinda katiba.Mwenyekiti wa chama hicho,Linus Kaikai, alilitaka bunge la sasa kudumisha uhuru wa vyombo vya habari.