Justin Muturi Apendekeza Kurekebishwa Kwa Katiba

Spika wa bunge la taifa Justin Muturi sasa anapendekeza kurekebishwa kwa katiba ili kuwateuwa bungeni wawaniaji urais wanaoshindwa kwenye uchaguzi. Spika anasema maarifa ya baadhi ya wanasiasa maarufu hapa nchini yanahitajika bungeni. Spika Muturi alisema katiba yapasa kurekebishwa ili kuwapa fursa wawaniaji urais wanaoshindwa kuchangia ujenzi wa taifa bungeni. Muturi hata hivyo alitetea wingi wa wabunge wa mrengo mmoja wa kisiasa bungeni akisema kwenye maongozi ya kidemokrasia, uchaguzi husababisha hali ya kuwepo walio na wengi na wachache bungeni. Aliyasema hayo katika eneo la Mbeere kaunti ya Embu huku baadhi ya wabunge wa Jubilee wakiwashtumu wenzao wa CORD na kutokuwa na nia njema ya kukomesha mzozo kwenye juhudi zinazoendelea za kurekebisha tume ya uchaguzi. Majuma mawili baada ya tume ya pamoja kuanza vikao vyake wabunge wa Jubilee wanadai hawajasikia malalamishi halali kutoka kwa wenzao wa muungano wa CORD dhidi ya tume ya IEBC. Kutokana na hali hiyo muungano tawala unadai kwamba wapinzani hawazingatii kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao.