Justice Jessie Lessit kuamua alhamisi iwapo gavana Obado ataachiliwa kwa dhamana

Jaji wa mahakama kuu Justice Jessie Lessit siku ya alhamisi ataamua iwapo gavana wa kaunty ya Migori Zachariah Okoth Obado ataachiliwa kwa dhamana. Hii ni baada ya mawakili wake, familia na upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wao.

Jaji aliagiza Obado ambaye ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Sharon Otieno azuiliwe katika gereza la eneo la viwandani. Mawakili Nicholas Ombijja na Cliff Ombetta waliiomba mahakama imuachilia huru kwa dhamana mshtakiwa wakisema mshukiwa atafika mahakamani atakapohitajika.

Walisema mteja wao tayari ameshtakiwa na kuhukumiwa na vyombo vya habari. Hata hivyo ukipinga ombi hilo la dhamana upande wa mashtaka ulisema mshtakiwa huenda akawatisha mashahidi na kuvurugha uchunguzi endapo ataachiliwa kwa dhamana.

Upande wa mashtaka ulisema maisha mawili yalipotezwa kinyama na ukamhimiza jaji kuzingatia hayo atakapokuwa akitoa uamuzi. Justice Lessit atatoa uamuzi tarehe 27 mwezi huu. Wasaidizi wa Obado Michael Juma Oyamo na Caspal Ojwang’ Obiero pia wameshtakiwa kwa mauaji.