Julius Karangi Ateuliwa Mwenyekiti Wa Halmshauri Ya Viwanja Vya Ndege

Rais Uhuru Kenyatta amemteuwa aliyekuwa mkuu wa majeshi jenerali mstaafu Julius Karangi kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya viwanja vya ndege hapa nchini kuanzia tarehe 24 Juni   mwaka huu hadi tarehe mosi Januari mwaka 2018 . Uteuzi wa Karangi umechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali lililotolewa leo ,ambalo pia lina majina ya watu wengine walioteuliwa na serikalini.  Karangi amechukua mahali pa aliyekuwa inspekta jenerali wa polisi  David Kimaiyo ambaye uteuzi wake umefutiliwa mbali. Kimaiyo aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya halmashauri hiyo mwezi Disemba mwaka  2014 baada ya kujiuzulu kama inspekta jenerali wa polisi kufuatia msururu wa mashambulizi ya kigaidi hapa nchini. Rais pia amemteuwa  Ronald Osumba aliyekuwa mgombea mwenza wa Peter Kenneth katika uchaguzi mkuu wa mwaka  2013 kuwa mwenyekiti wa bodi ya hazina ya vijana. Wanasiasa wengine kadhaa wakiwemo  Raphael Tuju, Noah Katana Ngala na  Ramadhani Kajembe pia wameteuliwa kuwa wenyeviti wa mashirika mbali mbali ya serikali.