Juhudi za kuchimbua manusura yarejelea Sierra Leone

Juhudi za kuwachimbua manusura inarejelewa katika mji mkuu wa Sierra Leone, baada ya maporomoko ya tope na mafuriko kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300. Makazi yao mjini Freetown yalifunikwa na maporomoko hayo baada ya sehemu ya mlima wa Sugar Loaf kuporomoka kufuatia mvua kubwa mapema jana asubuhi. Wengi wa waathiriwa walikuwa wangali wanalala mkasa huo ulipotokea. Makamu wa rais wa Sierra Leone Victor Foh ameonya kwamba idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka. Watu wengine elfu-3 waliachwa bila makazi wakati wa mkasa huo.