Jubilee yajizatiti kubadilisha mfumo wa upeperushaji matokeo ya uchaguzi

Chama cha Jubilee kinajizatiti kubadilisha mfumo wa upeperushaji matokeo ya uchaguzi ili kujumuisha mfumo mbadala wa kuwasilisha matokeo hayo kwa njia isiyo ya kidijitali kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais. Kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale aliwasilisha mswada huo bungeni leo ambao miongoni mwa mapendekezo mengine ni kuwa kamishna yeyote yule anaweza kutangaza matokeo ya ucahguzi wa urais ikiwa mwenyekiti au naibu wake hapatikani. Mswada huo pia unapendekeza kuwa ikiwa mgombeaji urais atajiondoa kutoka marudio ya uchaguzi wa urais, mgombeaji anayesalia anaweza kuapishwa kuwa rais. Wasimamizi wa uchaguzi wanaokosa kutia saini kwenye fomu za uchaguzi watafungwa vifungo vya miaka mitano gerezani ikiwa mswada huo utaidhinishwa. Duale alisema mswada huo unalenga kukabiliana na dosari zilizonukuliwa na mahakama ya juu kwa kusababisha kufutiliwa mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.