Jubilee yajitenga na rufaa ya kumng’oa jaji Maraga

Chama cha Jubilee kimejiepusha na rufaa iliyowasilishwa na mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu kwa tume ya kuajiri wahudumu wa idara ya mahakama ikitaka kuondolewa kwa jaji mkuu David Maraga. Wakiongea na wanahabari kenye majengo ya bunge, wanasiasa wa chama hicho wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale na seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen walithibitisha kuwa rufaa hiyo haikushinikizwa na viongozi wa chama hicho au kundi la wabunge wa chama. Wanasiasa hao waliwahimiza viongozi waliochaguliwa wa chama cha Jubilee kujiepusha na mambo yasiyo na umuhimu na badala yake kumpigia upatu rais Uhuru Kenyatta kwenye azma yake ya kuchaguliwa tena. Hata hivyo Murkomen alisema rufaa hiyo inaibua masuala muhimu yanayopasa kushughulikiwa kuhusiana na hatua ya mahakama ya juu ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe nane mwezi uliopiota. Hapo jana, Wambugu aliwasilisha rufaa kwa tume ya kuajiri wahudumu wa idara ya mahakama akitaka jaji Maraga aondolewe akidai ana ushahidi wa kubainisha kuwa alitekeleza mapinduzi ya idara ya mahakama pale alipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.