Jubilee itaendelea kutekeleza maendeleo Kilifi – Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali ya Jubilee itaendelea kutekeleza maendeleo kwa wakazi wa Kilifi na taifa lote kwa jumla. Rais alisema serikali ya Jubilee itaendelea kutekeleza maendeleo kote nchini ikiwa ni pamoja katika maeneo ambako wakazi wengi huangukia mtego wa maneno matupu ya upinzani. Rais alisema serikali ya Jubilee imejenga barabara nyingi zaidi katika historia ya nchi hii na itaendelea na kazi yake ya maendeleo katika muda wa miaka mitano ijayo. Huko Kilifi, rais na naibu wake William Ruto alitaja baadhi ya barabara ikiwemo barabara ya kutoka Kaloleni hadi Mavueni ambayo ujenzi wake umekamilika , barabara ya kutoka Mariakani hadi Bamba, ambayo inaendelea kujengwa na barabara ya kutoka Malindi hadi Sala Gate ambayo ujenzi wake unaendelea na ile ya kutoka Marafa hadi Sabaki. Viongozi hao pia walitaja uwekaji lami barabara zilizoko mjini Kaloleni kuwa sehemu ya miradi ambayo imetekelezwa kubadili taswira ya kaunti ya Kilifi. Rais alisema ana imani ya kumshinda mgombea uchaguzi wa upinzani na kura nyingi zaidi kwenye marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi huu.