Juan Martin del Potro alimshinda Roger Federer katika seti nne na kufuzu kwa nusu fainali

Mzaliwa wa Argentina Juan Martin del Potro alimshinda Roger Federer katika seti nne na kufuzu kwa nusu fainali ya mashindano ya tenisi ya US Open. Del Potro, anayeorodheshwa katika nafasi ya 24 mashindanoni, alimshinda Federer seti tatu kwa moja za 7-5, 3-6, 7-6, 6-4 na kufuzu kwa nusu fainali huku akiwaridhisha mashabiki wengi waliokuwa uwanjani. Del Potro sasa atachuana na Rafael Nadal wa Uhispania kwenye nusu fainali baada ya Nadal kumbandua Andrey Rublev wa Urusi. Ushindi wa Del Potro una maana kuwa Federer na Nadal wataendelea kusubiri kwa mwaka mwingine mmoja kuchuana kwenye mashindano ya US Open. Aidha Nadal, anayeorodheshwa wa kwanza mashindanoni, ataendelea kuorodheshwa wa kwanza duniani mbele ya Federer. Mechi ya pili ya nusu fainali itakuwa baina ya Kevin Anderson wa Afrika Kusini na Pablo Carreno Busta wa Uhispania.