Aliyejifanya polisi aidhinishwa kuwania ubunge Njoro

Joshua Waiganjo aliyejisingizia kuwa afisa wa polisi na ambaye alihudumu kifungo gerezani ameidhinishwa kuwania kwenye uchaguzi mkuu mwezi Agosti. Kwenye barua kwa msajili wa vyama vya kisiasa Lucy Ndunga��u, Waiganjo ametimiza masharti yote kabla ya kuruhusiwa kuwania kama mgombeaji huru. Licha ya kufungwa kwenye gereza la Naivasha Waiganjo anatumai kushinda kiti cha ubunge cha Njoro kwenye uchaguzi huo. Mahakama kuu ya Naivasha leo itatoa uamuzi kuhusiana na rufaa iliyowasilishwa na Waiganjo kupinga kifungo cha miaka mitano gerezani ambacho amekuwa akihudumu kwenye gereza hili tangu mwezi Oktoba mwaka 2015 baada ya kupatikana na hatia ya kujisingizia kuwa naibu kamishna wa polisi. Mwishoni mwa juma lililopita, Waiganjo alikuwa miongoni mwa wafungwa waliofuzu kwa cheti cha Diploma katika Theolojia kwenye gereza la Naivasha. Mpango huo ulifadhiliwa na kanisa la Presbyterian la Afrika mashariki.