Joseph Nkaissery ameaga dunia

Waziri wa usalama wa kitaifa Joseph Nkaissery ameaga dunia mapema Jumamosi; muda mfupi tu baada ya kulazwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu.

Kulingana na taarifa ya Ikulu ya Nairobi kwa vyombo vya habari, mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua amesema Nkaissery aliugua na akapelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu.

Serikali imeahidi kutoa habari kadri zinapochipuka kuhusu kisa hicho. Mnamo Ijumaa, Nkaiseri aliandamana na rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria mkutano wa kuombea amani wakati wa uchaguzi ulioandaliwa na muungano wa makanisa ya kievanjelisti katika uwanja wa Uhuru Park jijini Nairobi.

Nkaissery alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Kajiado ya Kati mwaka 2002 kwa tikiti ya chama cha KANU na kuchaguliwa tena mwaka wa 2007 na 2013 kwa tikiti ya chama cha ODM .

Jenerali Nkaissery amefariki akiwa na umri wa miaka 67. Mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee Funeral Home. Aliteuliwa kutoka upinzani kuwa waziri wa usalama wa kitaifa mwaka 2014 na kuchukua mahali pa Joseph Ole Lenku. Kabla ya kuingia katika ulingo wa siasa, Nkaiseri alihudumu kama kamanda wa chuo cha utoaji mafunzo kwa wanajeshi , naibu kamanda wa jeshi la nchi kavu, kamanda wa kikosi cha jeshi la nchi kavu, mkuu wa wafanyakazi wa jeshi la nchi kavu, naibu mkuu wa majeshi ya nchi kavu, na mwelekezi wa vita wa jeshi la nchi kavu.