Joseph Kinyua Kuongoza Mkutano Na IEBC

Mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua kesho ataongoza mkutano wa kamati ya idara mbali mbali za serikali na makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kujadili kuondoka kwao ofisini. Kamati hiyo iliyo na uwakilishi kutoka wizara ya fedha, Tume ya mishahara na marupurupu, Ofisi ya mwanasheria mkuu, wizara za usalama wa taifa na utumishi wa umma ilikutana leo na inatumai kuwa na makubaliano kamili kufikia tarehe 4 mwezi ujao. Msemaji wa serikali Eric Kiraithe amesema kamati hiyo itafanya mkutano wake wa kwanza na makamishna hao kesho kurahisisha kuondoka kwao kwa njia ya heshima na kuhakikisha mabadiliko katika tume hiyo. Serikali imesema kwamba inatambua dharura iliyopo ya mabadiliko na imejitolea kuharakisha mpango huo kuambatana na sheria huku wataalamu wa kisheria wakitahadharisha kuhusu ongezeko la hali isiyojulikana kuhusu swala hilo. Upinzani ulitisha kurejelea maandamano ya kuipinga IEBC ikiwa makamishna hao wa sasa hawataondoka ofisini kufikia mwisho wa mwezi huu wakilaumu baadhi ya taasisi kwa kutatiza mpango wa kuondoka kwao.