Joseph Kabila kuidhinisha sheria ya uchimbaji madini

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya demokrasia ya Kongo hivi karibuni ataidhinisha sheria mpya kuhusu uchimbaji madini. Tangazo hilo limejiri baada ya mazungumzo ya saa sita kati ya rais Kabila na wakurugenzi wa kampuni za uchimbaji madini mjini Kinshasa. Sheria hiyo itaashiria kuongezwa kwa ushuru na kuondoa kipengele kilichowakinga wachimbaji madini dhidi ya mageuzi kwenye mfumo wa malipo ya ushuru wa forodha na ada nyinginezo kwa kipindi cha miaka kumi. Mswada huo umepingwa vikali na wachimbaji madini. Kampuni ya Randgold inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Kibali Kaskazini Mashariki mwa Kongo ilisema mwezi jana kuwa itapinga sheria hiyo mpya na inataka kuwe na mashauriano zaidi kati ya pande husika. Serikali imepuuza madai kuwa sheria hiyo mpya ya madini itaziletea hasara kampuni hizo za uchimbaji madini.