Jopo Linalomchunguza Jaji Philip Tunoi Lahairisha Vikao Vyake Hadi Jumatatu

Jopo linalomchunguza jaji wa zamani wa mahakama ya juu Philip Tunoi jana liliahirisha vikao vyake hadi Jumatatu, ambapo litaamua iwapo jaji huyo alistaafishwa ki-halali. Hayo yanajiri juma moja baada ya mahakama ya juu kudumisha uamuzi wa mahakama ya rufani kwamba Ma-jaji wanapaswa kustaafu wakiwa na umri wa miaka 70. Uamuzi huo utabaini iwapo Jopo hilo litaendelea na vikao vyake vya kuchunguza mienendo ya jaji Philip Tunoi. Mwenyekiti wa Jopo hilo Sharad Rao alisema wataendelea na shughuli zao hata mwishoni mwa Juma na kutoa uamuzi wao mapema siku ya Jumatatu. AliongezaA� kwamba baada ya uamuzi wa siku ya Jumatatu, Jopo hilo litaamua iwapo wakili wa Tunoi, Fred Ngatia, atawasilisha hoja zake juu ya ushahidi uliowasilishwa kwao. Hayo yaliafikiwa baada ya wakili wa Tunoi Fred Ngatia na yule wa Jopo hilo, Paul Nyamodi, kuwasilisha hoja zao. Nyamodi alihoji kwamba Jopo hilo linapaswa kutamatisha shughuli zake kwa vile Jaji huyo amestaafishwa na tume ya kuajiri wafanyikazi wa Idara ya mahakama (JSC), kupitia kwa arifa yaA� tarehe 15 mwezi Juni. Ngatia, hata hivyo, alisema Jopo hilo linapaswa kuendelea na vikao vyake kwa vile Jaji huyo hakustaafishwa ki-halali. Alihoji kwamba ilani ya kustaafishwa kwa jaji huyo ilipaswa kutolewa na idara ya mahakama na wala sio tume ya kuajiri wafanyikazi wa idara ya mahakama (JSC) kuambatana na uamuzi uliotolewa na mahakama kuu mwaka 2014.